NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Isaya Mbenje na watendaji walio chini yake kujitafakari juu ya mwenendo wa utendaji kazi wao kutokana na kushindwa kusimamia miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo.
Mhe Ndejembi ametoa kauli hiyo leo alipotembelea miradi ya elimu ya msingi na sekondari inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo ikiwa ni maandalizi ya kupokea wanafunzi wa mwaka mpya wa masomo 2024
Katika ziara yake, Mhe Ndejembi ameonesha kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Pangani Halisi iliyogharimu kiasi cha Sh. Bilioni Moja, Shule ya Sekondari Masiaka inayojengwa kupitia mradi wa SEQUIP inayogharimu Sh. Milioni 585 na Shule ya Msingi Bushiri iliyogharimu Sh. Milioni 440 ikijengwa kupitia mradi wa BOOST.
Amesema Shule ya Pangani Halisi ilipaswa iwe imeshakamilika lakini mpaka sasa ujenzi huo haujakamilika huku halmashauri ikiwa imeishiwa fedha ikilinganishwa Shule ya Masiaka ambayo imepata sh. Milioni 580 majengo yake yapo kwenye hatua kubwa na inaendelea na ujenzi.
“Ofisi ya Rais-TAMISEMI chini ya Waziri Mhe Omary Mchengerwa hatutomchekea yeyote anayechezea fedha za umma, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na wasaidizi wako mjitafakari kwa sababu hawamsaidii kazi Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika ngazi ya huku chini kuna tatizo la usimamizi wa miradi na kutojali fedha zinazoletwa kutekeleza miradi hii. Sasa kwa TAMISEMI hii hatuwezi kuja tukakuta usimamizi mbovu wa miradi tukashindwa kuchukua hatua,”amesema.
0 Comments