Na, Mwandishi wetu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza bendera ya taifa kupepea nusu mlingoti kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa.
Lowassa amefariki mnamo Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKIC) alipokuwa anapata matibabu ya mapafu na shinikizo la damu.
Aidha katika taarifa yake kwa Taifa, aliyoitoa kupitia Televisheni ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), akiwa Arusha, Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango alisema kuwa Lowassa amekuwa JKCI tangu Januari 14, 2022 baada ya kurejea nchini kutoka Afrika ya Kusini alipokuwa anapokea matibabu ya maradhi hayo.
Kufuatia hilo ilimlazimu Dkt. Mpango kukatisha safari yake ya kikazi wilayani Longido, Mkoani Arusha na kuelekea Wilayani Monduli kutoa taarifa hiyo.
“Rais ametangaza siku tano za maombolezi ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti, kuanzia leo Februari 10, 2024, taarifa zaidi kuhusu msiba huu zitaendelea kutolewa na Serikali” Amesema Dkt, Mpango.
Ikumbukwe kuwa mwishoni mwa mwaka 2022, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimtembelea Lowasa nchini Afrika ya Kusini ambapo alikuwa anapatiwa matibabu kabla ya kurejea Nchini akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenda kumjulia hali Waziri Mkuu huyo wa zamani.
0 Comments