Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Ad Code

MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA NA DAWA ZA KULEVYA YASHIKA KASI

   

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imehitimisha mafunzo kwa Maafisa waelimishaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU} kutoka katika mikoa na wilaya zote nchini, yaliyofanyika kwa lengo la kujengeana uwezo na kupeana mbinu zaidi za uelimishaji Umma katika mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya nchini . 

Akizungumza jana jijini Dodoma wakati wa kufunga mafunzo kuhusu mkakati wa habari, elimu na mawasiliano, programu ya TAKUKURU rafiki na tatizo la dawa za kulevya na mapambano dhidi ya rushwa kwa maafisa wanaohusika na uelimishaji Umma na mawasiliano, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, tatizo la dawa za kulevya na vitendo vya rushwa ni tatizo mtambuka linalohitaji ushiriki wa pamoja katika kukabiliana nalo. 

“Yapo mahusiano makubwa kati ya vitendo vya rushwa na biashara ya dawa za kulevya, kwani kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara ya dawa za kulevya hutumia rushwa kufanikisha uhalifu wao. Hivyo, ili kuhakikisha tunapinga vitendo vya rushwa na dawa za kulevya, tumeona ni vema elimu juu ya rushwa na dawa za kulevya ikatolewa pamoja” ,amesema Lyimo.

Ameongeza kuwa, Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ziliingia makubaliano ya kutumia klabu za rushwa zilizopo shuleni na vyuoni kutoa elimu kuhusu rushwa na dawa za kulevya ili kuwafikia walengwa kwa urahisi na kutumia rasilimali chache za serikali hali itakayoleta tija zaidi katika kujenga uzalendo kwa vijana kuchukia vitendo vya rushwa na dawa za kulevya.

“Tumeshuhudia maafisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wakishirikiana kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya kijamii nchini hali ambayo itasaidia kuongeza uelewa juu ya athari za ya rushwa na matumizi na biashara ya dawa za kulevya” amesema Lyimo. 

Aidha, Kamishna Jenerali Lyimo ametoa wito kwa wadau wote kutambua kwamba elimu ni moja nyenzo muhimu ya kukabiliana na changamoto ya dawa za kulevya na rushwa. Hivyo, maafisa wa DCEA, maafisa wa TAKUKURU, wakuu wa shule na vyuo, walimu, walezi wa vilabu, vyombo vya habari, wasanii, vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi wote washirikiane katika kupinga rushwa na dawa za kulevya.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi mkuu wa Takukuru Bi. Neema Makalyelye amesema matunda ya mafunzo haya yataonekana katika utendaji kazi wa waelimishaji wetu mara watakaporejea katika vituo vyao vya kazi. 

“Katika siku tatu za mafunzo washiriki waliweza kujifunza kuhusu tatizo la dawa za kulevya, makundi ya dawa za kulevya, sababu za matumizi, namna ya kumtambua mtumiaji wa dawa za kulevya, kuzitambua dawa tiba zenye asili ya kulevya, uraibu wa dawa za kulevya, magonjwa ambukizi, na tiba saidizi kwa kutumia dawa, namna ya kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na  uwepo wa huduma katika nyumba za upataji nafuu” Amesema Mwakalyelye.

Ameongeza kuwa, washiriki wamepitishwa katika andiko maalum la kampeni ya kutokomeza rushwa na dawa za kulevya katika shule na vyuo nchini, muongozo wa utoaji elimu kuhusu rushwa na dawa za kulevya shuleni na vyuoni, na kuelimishwa kuhusu uhusiano uliopo kati ya dawa za kulevya na rushwa ili waweze kutumia nyenzo hizo katika vituo vyao kufanya kazi. 

“Ni matarajio yetu kuwa, mafunzo haya yataleta mabadiliko chanya katika utendaji kazi na hatimaye kuifanya jamii ya kitanzania kuichukia rushwa na dawa za kulevya kwani hivi vyote vina madhara kwa mtu, jamii na taifa kwa ujumla” ameongeza Mwakalyelye.

Ushirikiano wa DCEA na TAKUKURU ni utekelezaji wa agizo la serikali kupitia kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) kuzitaka taasisi hizi kuunganisha nguvu katika kutoa elimu juu ya athari za vitendo vya rushwa na biashara ya dawa za kulevya kwa kuweka mkazo kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuoni kupitia klabu za kupinga rushwa ambazo tayari zimeanzishwa na TAKUKURU.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com

Post a Comment

0 Comments